Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa Mjini Magharibi imeanzisha operesheni maalum katika Shehia zote 121 za Mkoa huo ya kuwakamata watu wanaofanya vitendo vya uporaji, wizi na uhalifu.
Akitoa taarifa kuhusu operesheni hiyo, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amesema operesheni hiyo itafanywa na vikosi vyote vya ulinzi ili kuwatia mikononi wale wote wanaojihusisha na matendo hayo pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria.
Mkuu wa Mkoa amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ina dhima ya kusimamia suala zima la ulinzi ndani ya Mkoa huo hivyo ameonya kuwa haitachelea kumchukuli hatua mtu yoyote yule atakaebainika kujihusisha na uporaji, wizi na uhalifu wakati operesheni hiyo ikiendelea.
Ametanabahisha kuwa Serikali ina vyanzo vya kutosha kuweza kupata taarifa za vijana wanaofanya vitendo hivyo na kuwataka wazazi na walezi kuwaelimisha vijana wao kutojiingiza kwenye vitendo hivyo badala ya kuwalinda.
Aidha Idrissa amewataka pia Masheha na jamii kutoa mashirikiano yao katika operesheni hiyo kwa kutoa taarifa za watu wanaofanya matendo hayo na kusema kuwa vyombo vya ulinzi itawahifadhi wale wote watakaotoa taarifa hizo.
Kwa upande mwengine Mkuu wa Mkoa amewaasa vijana kutojiingiza kwenye vitendo vya aina hiyo kwani havina tija hata kidogo kwao, familia zao na taifa kwa ujumla.
Hata hivyo amewahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kusimamia suala zima la amani na utulivu ndani ya Mkoa huo ili waweze kuendelee na shughuli zao za maisha kama kawaida.