Uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi umesema kwamba utaendelea kufanya kazi kwa karibu na taasisi zenye lengo la kuisaidia jamii.
Katibu Tawala Mkoa Mjini Magharibi Moh’d Ali Abdalla amesema hayo wakati akizindua mradi wa miaka minne(2023-2027) wa “Kizazi Hodari”, wenye lengo la kuwasaidia watoto waliyoathirika na visusi vya UKIMWI na wanaoishi katika mazingira magumu kwenye Shehia 21 za Wilaya ya Mjini.
Amewakata watendaji wa Mkoa huo na Wilaya watakaosimamia mradi huo kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao ipasavyo ili kuona malengo ya mradi yanafikiwa.
Katibu huyo ameeleza pia Mkoa una matumaini makubwa kwamba taasisi ya Deloitte na Jumuia ya ZAMWASO wanaotekeleza mradi huo wataweza kuwafikia walengwa wakiwemo watoto wote wanaoishi na VVU na wenye mazingira magumu katika Shehia zote zilizokusudiwa.
Aidha Moh’d amelishukuru Shirika la Msaada la Watu wa Marekani la USAID kwa ufadhili wa mradi huo pamoja na miradi mingine inayoendelea kutekelezwa ndani ya Mkoa Mjini Magharibi ambayo inagusa makundi mbali mbali na kuongeza kuwa Serikali inathamini sana misaada hiyo.
Naye Mratibu Huduma za Kuzuia Maambukizi ya VVU kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Khadija Abbas Mohamed amesema watakuwa wakifuatilia utekelezaji wa programu ya “Kizazi Hodari” ili kuhakikisha inafuata miongozo na taratibu katika shughuli zao.
Meneja wa Mradi kutoka Jumuia ya kuwasaidia wanawake wanaoishi na VVU ZAMWASO, Halima Salum Kheri amesema kupitia programu mbali mbali zilizotekelezwa na Jumuia hiyo zaidi ya wanawake 300 waliopata elimu ya ujasiriamali wameweza kujitegemea pamoja na vijana waliopewa elimu ya amali kuweza kujiajiri wenyewe.