Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepongewa kwa ujenzi wa miradi mikubwa ya Maendeleo katika Mkoa Mjini Magharibi.
Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa matangi ya maji huko Kama, Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru 2023 Abdallah Shaib Kaimu ameeleza kuridhishwa na kazi iliyofanywa katika mradi huo.
Ameitaka Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha miradi hiyo inajengwa katika kiwango kinachotakiwa na kukamilika kwa wakati.
Ameongeza kwa kusema kwamba miradi hiyo inatumia fedha nyingi za Serikali hivyo ni muhimu kuona inaleta manufaa kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘A’ Suzan P. Kunambi ameahidi kuwa wataendelea kufuatilia ujenzi wa miradi kwenye Wilaya yake na hatosita kuchukua hatua dhidi ya wakandarasi watakaojenga chini ya kiwango.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini Mhe. Machano Othman Said ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa mradi huo mkubwa na kusema unakwenda kuondosha tatizo la maji kwa wananchi wa Jimbo lake.
Akiwa katika mradi huo Kiongozi pamoja na wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa walikagua ujenzi sambamba na kupitia nyaraka zake mbali mbali kabla ya kuweka jiwe la msingi.