OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Masheha watakiwa kuwatambua wahamiaji.
HabariHabari Mpya

Masheha watakiwa kuwatambua wahamiaji.

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amewataka Masheha wa Mkoa huo kushirikiana na Jeshi la Uhamiaji katika kuwatambua wageni wanaoishi kwenye maeneo yao bila kufuata sheria na taratibu za nchi.

Akifungua kikao kazi kuhusu masuala ya uhamiaji kwa Masheha wa Wilaya ya Mjini kilichofanyika Makao Makuu ya Jeshi la Uhamiaji Zanzibar,  amesema Masheha wanawajibu wa kufuatilia kwa karibu wageni wanaohamia kwenye maeneo yao ili kudhibiti wahamiaji haramu.

Amesema kumekuwa na idadi kubwa ya wageni wanaoingia kwenye Mkoa huo kwa shughuli mbali mbali zikiwemo za kiuchumi, hivyo ni lazima wahakikishe wahamiaji hao wanafuata sheria badala ya kuwaacha kuishi kwenye maeneo yao kiholela.

Mkuu huyo wa Mkoa ameupongeza uongozi wa Jeshi la Uhamiaji Zanzibar kwa kuandaa kikao hicho na  kusema kuwa kitaweza kuwasaidia Masheha kuongeza uelewa katika kuyafanyia kazi mambo yanayohusu uhamiaji.

Kamisha wa  Uhamiaji Zanzibar Hassan Ali Hassan amesema kumekuwa na changamoto kubwa ya wahamiaji wanaoingia nchini kutoka nchi za jirani na baadhi yao wamekuwa wakifanya udanganyifu wa kupata vitambulisho vya uraia vinavyotumika nchini.

Amesema Jeshi la uhamiaji limeona kuna haja ya kuwapatia elimu  Masheha hao kwa vile wataweza kusaidia kuwatambua  na kuwapatia taarifa za watu wanaohamia kwenye maeneo yao.

Kwa upande wao Masheha wameahidi kuyafanyia kazi mafunzo waliyoyapata katika kikao na wameiomba jamii kutoa mashirikiano yao yatakayoweza kufanikisha suala hilo.