Mkuu wa mkoa Mjini Magharibi Idrissa kitwana Mustafa amewataka Masheha wa Mkoa huo kuwa waadilifu katika kutekeleza majukumu yao pamoja na kuondoa changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi wa Shehia zao
Ameyasema hayo mara baada ya kuwaapisha masheha wa Shehia mbali mbali aliyowateua hivi karibuni, hafla iliyofanyika huko Afisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Vuga.
Amesema kuwa bado kuna kunachangamoto kadhaa katika Shehia zao ikiwemo suala la uhalifu ,wizi , rushwa na vitendo vya udhalilishaji na kuwataka kuchukua hatua za makusudi kupambana na mambo hayo.
Mkuu wa Mkoa amewataka masheha hao pia kuachana na masuala ya migogoro ya ardhi na kutojihushisha katika migogoro hiyo na kusema kuwa hatasita kuchukua hatua dhidi ya Sheha yoyote atakaebainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Kwa upande mwengine amewataka Masheha hao kutoa huduma kwa wananchi bila ya ubaguzi wa aina yoyote na kutofanya upendeleo katika kutoa huduma muhimu kwa jamii.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa Mjini Magharibi Radhiya Rashid Haroub amewakumbusha Masheha kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, mwongozo na taratibu za kazi zao.
Jumla ya Masheha wa Shehia saba waliapishwa ikiwemo Mlandege, Shaurimoyo, Mwembeladu, Mwakaje, Welezo, Kianga na Kombeni na kukamilisha safu wa Masheha wa Shehia zote 121 za Mkoa huo.