OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Dkt.Mwinyi awanasihi wafanyabiashara kutopandisha bei za vyakula.
HabariHabari Mpya

Dkt.Mwinyi awanasihi wafanyabiashara kutopandisha bei za vyakula.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Ali Mwinyi leo Jumatatu tarehe 26-2-2024 amefanya ziara maalum kutembelea masoko mbali mbali na Bandari ya Malindi Mkoa wa Mjini Magharibi.

Lengo la ziara yake hiyo ni kuzungumza na wafanyabiashara pamoja na uongozi wa Bandari zikiwa zimebaki takriban wiki mbili kabla ya kuanzia mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Akizungumza katika Soko la Jumbi, Darajani na Soko la Samaki Malindi Dkt. Mwinyi amewanasihi wafanyabiashara kutopandisha bei za bidhaa katika kipindi hiki.

Aidha amewataka wafanyabiashara  kutoutumia mwezi huo kama mwezi wa kupata faida zaidi jambo ambalo  limekuwa likiwaumiza wananchi hasa wanyonge.

Dkt. Mwinyi amewafahamisha wafanyabiashara hao kuwa hakuna sababu ya kuongeza bei za vyakula vinavyozalishwa hapa nchini pamoja na  Samaki kwani bidhaa hizo hazina kodi ambayo ingepelekea kupanda kwa gharama.

Rais wa Zanzibar amesema pia Serikali imeondoa kodi ya thamani VAT kwa bidhaa muhimu kutoka nje ikiwemo mchele, unga, sukari na mafuta ili wananchi waweze kumudu kununua bidhaa hizo na kusema kuwa Serikali haitasita kuwafutia leseni waingizaji chakula  watakaoshindwa kufuata bei elekezi iliyopangwa na Serikali.

Akijibu lalamiko la mmoja wa wafanyabiashara juu ya kupanda kwa bei ya ng’ombe kutoka Bara, Dkt. Mwinyi amesema Serikali itazungumza na sekta husika ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuangalia namna ya kupunguza gharama.

Kadhalika Dkt. Mwinyi ameuagiza Mkoa, Baraza la Manispaa Mjini na Mamlaka ya Uhifadhi wa Mji Mkongwe kutowabughudhi wafanyabiashara wadogo wadogo  katika maeneo ya Mjini na badala yake wawawekee mazingira na utaratibu mzuri wa kufanya shughuli zao.

Akiwa Bandari kuu Malindi  Rais wa Zanzibar alipokea taarifa kutoka uongozi wa Shirika la Bandari Zanzibar kuhusu hatua mbali mbali wanazochukua kuharakisha ushushaji wa bidhaa.

Nae Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dkt.Khalid Salum Mohammed alisema meli zote zitakazoingia nchini  na  bidhaa kwa ajili  mwezi Mtukufu wa  Ramadhani na Sikukuu ya Eid el Fitri zitapewa kipaumbele kushusha mizigo ili uweze kuingia sokoni.