Taasisi ya Mpango wa Hiari wa Nchi za Afrika Kujitathmini kwa Vigezo vya Utawala Bora APRM imeshauriwa kushuka kwa wananchi kwa ajili ya kutoa elimu ili kuweza kuzifahamu kazi zinazofanywa na Taasisi hiyo.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa alipokuwa akizungumza na ujumbe wa taasisi hiyo ukiongozwa na Katibu Mtendaji wa APRM Lamau Mpolo ulipofika Ofisini kwake Vuga kujitambulisha.
Amesema kuwa wapo watu katika jamii wataweza kutoa maoni na mchango mzuri wakati watakapokuwa wakikusanya maoni kuhusu tathmini ya hali ya utawala bora nchini, hivyo ni vyema kushuka kwao pamoja na kutumia vyombo vya habari kutoa elimu juu ya malengo na kazi za taasisi hiyo kabla ya zoezi hilo kuanza.
Mkuu wa Mkoa ameihakikishia APRM kuwa Serikali ya Mkoa, Wilaya na Mabaraza yake ya Manispaa watatoa kila aina ya mashirikiano wakati zoezi hilo la tathmini litakapofanyika ili kuona lengo lililokusudiwa linafikiwa.
Aidha amesema kuwa Serikali inaamini chombo hicho itaifanya kazi hiyo kwa weledi na kuzingatia uzalendo kwa vile ripoti ya tathmini hiyo itazisaidia Serikali zote mbili kuweza kuangalia ni maeneo gani ambayo yanahitaji kuboreshwa kiutendaji pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananachi.
Nae Katibu Mtendaji wa APRM Lamau Mpolo ameyataja baadhi ya maeneo ambayo yataangaziwa katika Ripoti ya Pili ya Tathmini ya Utawala Bora Nchini kuwa ni suala la demokrasia, masuala ya kiuchumi namna yanavyoratibiwa pamoja na sekta binafsi namna zinavyowajibika kwa wananchi.
Ametaja maeneo mengine kuwa ni namna Serikali zinavyotoa huduma kwa wananchi na utayari wa kukabiliana na majanga mbali mbali yatokanayo na tabia nchi.
Lamau amesema kuwa mpango huo ni shirikishi hivyo ni muhimu kwa wadau mbali mbali kuwaunga mkono katika kazi hiyo ili waweze kufikia malengo ya APRM.
Sambamba na hayo amezipongeza Serikali zote mbili kwa juhudi wanazokuchukua katika kutatua changamoto mbali mbali zilizomo katika maeneo watakayoyafanyia tathmini.