Rais Mstaafu wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein ameisisitiza Wizara ya Afya kusomesha vijana wa fani mbali mbali katika sekta ya afya Ili kupata wataaamu wengi zaidi watakaoweza kuitumikia nchi yao.
Akizungumza mara baada ya kufungua Hospitali ya Wilaya ya Magharibi ‘A’ iliopo Mbuzini, Dkt. Shein amesema Hospitali za Wilaya na Mkoa zilizojengwa Unguja na Pemba lazima ziwe na madaktari bingwa wazalendo wenye uwezo wa kutoa matibabu bora kwa wananchi.
Amesema bado idadi ya vijana wanaosomeshwa na Serikali elimu ya juu ngazi ya Shahada na Shahada ya Uzamili katika fani ya udaktari ni wachache, hivyo ameitaka Wizara hiyo kuzitumia fursa zinazopatikana katika vyuo vya ndani na nje ya nchi kuwapeleka vijana wenye sifa ili kusomea taaluma hiyo.
Akizungumzia kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Shein amesema waasisi wa Mapinduzi wakiongozwa na Jemedari Marehemu Mzee Abeid Amani Karume walilazimika kufanya Mapinduzi hayo ili watu wa Zanzibar waweze kuwa huru wa kuendesha mambo yao wenyewe.
Dkt.Shein amefahamisha kuwa Mapinduzi hayo yalifanyika baada ya kutafuta uhuru wa njia ya demokrasia kuondoa utawala uliokuwepo kushindikana.
Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazurui amesema Serikali inaendelea kutekeleza mipango yote iliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Saba ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Binguni, ukarabati wa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja na Hospitali za Mikoa kwa lengo lile lile la kuinua sekta ya afya nchini.
Amesema Serikali inatarajia kuanzia ujenzi wa majengo mapya na ukarabati mkubwa wa Hospitali ya Mnazi Mmoja mwezi Aprili 2024 na mipango inaendelea kwa ujenzi wa Hospitali kubwa ya Kisasa Binguni na ujenzi Hospitali nyengine za Mikoa.
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa akitoa salamu kwa niaba wa wananchi wa Mkoa huo ameushukuru uongozi wa Wizara ya Afya kwa namna wanavyoshirikana na Mkoa pamoja na Wilaya zake katika masuala mbali mbali yanayohusiana na sekta hiyo.
Naye Kaimu Katibu Mkuu na Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Amour Suleiman Mohammed amesema jumla ya shilingi 8.8 bilioni zimetumika katika mradi huo ambapo shilingi bilioni 6.3 zimetumika kwa ujenzi wa Hospitali na shilingi Bilioni 2.5 zimetumika kwa ununuzi wa vifaa vya matibabu na gari ya kuchukulia wagonjwa.
Hospitali ya Wilaya ya Magharibi ‘A’ imeanza kutoa huduma zake tangu mwezi Oktoba 2023 ambapo kwa sasa wananchi wapatao 320,000 wa Wilaya hiyo wanapata matibabu mbali mbali kwenye Hospitali hiyo ikiwemo uchunguzi wa maradhi, upasuaji, wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU), uzazi, wagonjwa wa nje na wale wanohitaji kulazwa.