Uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi umesema kuwa Serikali imekuwa ikiutumia utulivu wa kisiasa uliopo nchini kuwalelea maendeleo wananchi wake.
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amesema hayo alipokuwa na mazungumzo na ujumbe kutoka Ubalozi wa Marekani Nchini Tanzania ukiongozwa na Mkuu wa Idara ya Siasa na Uchumi Jonathan Howard walipofika ofisini kwake Vuga kwa ajili ya kujitambusha pamoja na kuzungumzia masuala hayo.
Amesema kuwa kutokana na wananchi wa Mkoa huo kuwa kitu kimoja bila kujali itikadi zao za kisiasa, Serikali imefanikiwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo yenye azma ya kuimarisha huduma muhimu za kijamii.
Aidha ameongeza kuwa katika kuimarisha umoja miongoni mwa vyama vya vya siasa, Serikali ya Mkoa huo imeendelea kuwashirikisha viongozi wa vyama vya siasa katika matukio mbali mbali ya kimkoa na kitaifa yanayofanyika ndani ya Mkoa Mjini Magharibi.
Akizungumzia suala la uchumi Mkuu huyo wa Mkoa amesema Serikali imekuwa ikichukuwa juhudi kwa kuwawezesha wananchi kiuchumi, kuwajengea mazingira mazuri ya kibiashara pamoja na shughuli zao nyengine za kujipatia kipato.
Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Mkoa huo ameueleza pia ujumbe huo kuwa suala la uwepo wa amani na utulivu ndani ya Mkoa litaendelea kupewa kipaumbele ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kimaisha bila ya hofu yoyote.
Naye Mkuu wa Idara ya Siasa na Uchumi kutoka Ubalozi wa Marekeni Jonathan Howard amemueleza Mkuu wa Mkoa kuwa lengo la ujio wao mbali na kujitambulisha vilevile ni kuangalia namna watakayoweza kufanya kazi pamoja Serikali ngani ya Mkoa katika masuala yanayoihusu jamii.
Ameongeza kuwa Mkoa huo una zaidi ya asilimia 47 ya wakaazi wote wa Zanzibar hivyo unahitaji kuwa na mipango mizuri katika suala la uchumi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake.
Vilevile ameeleza kuvutiwa kwake na mashirikiano aliyoyaona miongoni mwa wananchi katika mikoa yote aliyoiyembelea hapa Zanzibar.