OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Mkoa wapata mafanikio ujenzi wa miradi ya maendeleo
HabariHabari Mpya

Mkoa wapata mafanikio ujenzi wa miradi ya maendeleo

Serikali ya Mkoa Mjini Magharibi imeeleza kupata mafanikio  makubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya awamu ya nane.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa alipokuwa akizungumza na ujumbe wa Wastahiki Meya na Madiwani wa Halmashauri za Mkoa wa  Kilimanjaro walipofika afisini kwake Vuga kumsalimia.

Ameitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa Hospitali za Wilaya na Mkoa, Skuli za horofa za msingi na Sekondari, majengo ya wajasiriamali na miundo mbinu ya maji na barabara.

Aidha amesema kuwa katika kipindi hicho Serikali imefanikiwa kuwapatia wavuvi boti na zana za kufanyia kazi pamoja na kuwawezesha wajasiriamali wadogo wadogo  kwa mikopo isiyo na riba ili kukuza biashara zao.

Mkuu huyo wa Mkoa amewaeleza viongozi hao kuwa Mkoa wake unatarajia kupata mafanikio makubwa zaidi katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ambapo kwa sasa miradi  kadhaa ujenzi wake umekuwa ukiendelea kwa kasi yakiwemo majengo ya Skuli, masoko , mradi mkubwa wa maji wa EXIM  na ujenzi wa barabara mpya katika Mkoa huo.  

Amewafahamisha kuwa Mkoa wake unajivunia maendeleo yanayoletwa na Viongozi Wakuu wa Nchi Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa pande zote mbili Muungano.

Akitoa shukrani kwa niaba ya viongozi wenzake, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Dkt. Saleh Nkwizu amesema kwamba miradi waliyoitembelea kwenye Manipaa tatu za Mkoa Mjini Magharibi imeonesha ni jinsi gani viongozi wa Viongozi Wakuu wa  Nchi walivyo imara kuhakikisha wanaitekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Amesema mafanikio hayo yanadhihirisha kuwa CCM itaendelea kushika hatamu na kuongoza Nchi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Awali viongozi hao  walifanya ziara katika Manispaa ya Magharibi ‘A’, Magharibi ‘B’ na Mjini kuangalia miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye Manispaa hizo.