OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>ZAHLIFE watakiwa kuwa wabunifu.
HabariHabari Mpya

ZAHLIFE watakiwa kuwa wabunifu.

Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya juu Zanzibar (ZAHLIFE), limetakiwa kuwa wabunifu ili kuleta mabadiliko yenye tija katika Shirikisho hilo.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya ZAHLIFE Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa alipokutana na uongozi mpya wa Shirikisho hilo ulipofika Ofisini kwake Vuga kwa ajili ya kujitambulisha.

Amewafahamisha kuwa endapo watakuwa wabunifu pamoja na kujifunza kutoka Shirikisho la Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), wataweza kufanya mambo mengi kwa manufaa ya Shirikisho lao na wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu hapa Zanzibar.

Aidha amewaeleza viongozi hao kuwa wamebeba dhamana ya kusimamia masuala ya wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu hapa Zanzibar, hivyo wanawajibu wa kufanya kazi zao kwa mashirikiano katika kipindi chote cha uongozi wao.

Mkuu wa Mkoa ameliahidi Shirikisho hilo kuwapa mashirikiano ili kufanikisha mpango wao wa kupata kiwanja pamoja na ujenzi wa jengo la ZAHLIFE.

Akitoa shukrani kwa niaba ya viongozi wenzake,Katibu wa Seneti  ya Viongozi wa Serikali za Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar Hamid Shaaban Khamis amesema kwamba uongozi mpya wa ZAHLIFE umejipanga kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazowakabili.