Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuzindua rasmi kituo cha biashara cha Darajani Souk siku ya Jumaamosi ya tarehe 18/02/2023.
Taarifa rasmi juu ya uzinduzi wa kituo hicho imetolewa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusiana na uzinduzi wa mradi huo hapo Darajani.
Amesema ujenzi wa kituo hicho cha kisasa chenye maduka 452, bustani na eneo la kuegesha magari tayari umeshakamilika na matayarisho mbali mbali ya uzinduzi wake yanaendelea vizuri.
Mkuu wa Mkoa amewaomba wananchi wa Mkoa Mjini Magharibi na Mikoa mengine jirani kuhudhuria kwa wingi kwenye uzinduzi wa mradi huo ambao amesema mbali na kubadilisha mandhari ya eneo la Darajani vile vile utatoa fursa nyingi zaidi kwa wafanyabiashara kuendesha shughuli zao.
Amesema kwamba tayari mpango mzuri wa kuendesha biashara umeshapangwa ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa mbali mbali zitakazouzwa katika kituo hicho yakiwemo mavazi, vifaa vya kiektroniki na huduma nyenginezo.
Mhe. Idrissa amewahakikishia wafanyabishara waliokuwepo kabla ya ujenzi huo kuwa watarudi kuendesha biashara zao mahala hapo na nafasi zitakazobaki watapewa wafanyabiashara wengine waliyoomba kukodi milango ya biashara kwenye eneo hilo.
Aidha Mkuu wa Mkoa amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa maelekezo yake yaliyopelekea kufanikisha ujenzi wa mradi huo katika eneo hilo la Darajani.
Ujenzi wa Darajani Souk uliogharimu kiasi ya shilingi bilioni nane ulianza mwezi februari mwaka 2022 huku awamu ya pili ya mradi huo ikitarajiwa kuanza hivi karibuni na kukamilika mwishoni mwa mwaka 2023.