OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Ziara ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi kukagua ujenzi wa miradi ya maendeleo kupitia fedha za COVID
HabariHabari Mpya

Ziara ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi kukagua ujenzi wa miradi ya maendeleo kupitia fedha za COVID

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amezitaka Kampuni zilizopewa  kazi ya ujenzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo kupitia fedha za COVID katika Mkoa huo kuhakikisha kuwa miradi  hiyo inakamilika kwa wakati na viwango vinavyokubalika kwa mujibu wa mikataba ya ujenzi.

Agizo hilo amilitoa wakati alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa miradi hiyo ikiweno ya Hospitali za Wilaya, Skuli na maeneo yatakayojengwa majengo ya wajasiriamali katika Wilaya ya Maghariboi A na Magharibi B pamoja na ujenzi wa Soko la Jumbi unaojengwa kwa mashirikiano baina ya Serikali na Mwekezaji.

Akiwa katika maeneo mbali mbali wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa amewaeleza Wahandisi wanaosimamia ujenzi wa miradi  kuwa  Serikali inataka  ujenzi wake uwende kwa kasi na kwa kuzingatia viwango, hivyo  hatarajii  kuona miradi hiyo ikijengwa chini ya kiwango au ikikwama kwa visingizio mbali mbali.

RC Kitwana akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Jumbi

Aliongeza kuwa Serikali ina amini kuwa Kampuni  za ndani na kigeni zilizopewa kazi hiyo pamoja na Kikosi cha Kujenga Uchumi (JKU), wanazo sifa na uwezo mkubwa, hivyo aliwataka kujenga miradi hiyo kwa ufanisi na kuikamilisha kwa wakati ili kuweza kuishawishi Serikali kuwapa ujenzi wa miradi mingine.

“lengo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ni kuona miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta ya elimu, afya na huduma nyengine muhimu”, alisema Idrissa.

Akizungumzia suala la ajira, Mkuu wa Mkoa amezisisitiza Kampuni hizo za ujenzi kuhakikisha wanawapa nafasi za kazi vijana na wanawake wa maeneo ya karibu na ujenzi wa miradi hiyo kwa kazi yeyote  ambayo haihitaji utaalamu pamoja na kuwalipa mishahara  kwa mujibu wa makubaliano yao.

Aidha amezitaka pia Kampuni hizo kutosita kuwasiliana na uongozi wa Wilaya na Mkoa iwapo kutatokea changamoto zozote zile wakati ujenzi ukiendelea ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa kushirikiana na sekta husika.

Mkuu wa Mkoa amewahimiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mabaraza ya Manispaa kufuatilia mara kwa mara maendeleo ya ujenzi na kuwataka pia wananchi kuwa walinzi wa miradi hiyo ili kuepusha vitendo vya wizi katika maeneo ya ujenzi.

Kwa upande mwengine Mkuu wa Mkoa alitoa wito kwa wananchi na wajasiriamali watakaopata mikopo isiyo na riba kupitia fedha za COVID kutumia vizuri fursa hiyo ili kuimarisha biashara zao.

“Rais wa Zanzibar ametafuta namna ya kupata fedha ili kuwakopesha wananchi na wajasiriamali wadogo mikopo isiyo na riba na vilevile kuwajengea masoko ya kufanya biashara zenu, kwa hiyo zitumieni vizuri fursa hizo”, alisema Idrissa.

Amesema juhudi hizo zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025, pamoja na ahadi zake alizozitoa wakati wa Kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.

Amewataka wananchi wa Mkoa wake kuendelea kumuunga mkoa na kumpa moyo Rais wa Zanzibar dhidi ya maono yake ya kuwaletea maendeleo  wananchi wa Zanzibar, na kuwataka kutosikiliza maneno ya watu  wanaobeza ujenzi wa miradi hiyo mikubwa unaoendelea hapa nchini.

Wakitoa shukurani zao kwa Mkuu wa Mkoa kufuatia ziara yake hiyo, Wakuu wa Wilaya  hizo wamemuahidi Mkuu  wa Mkoa kuwa wataendelea kufatilia kwa karibu maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo ndani ya Wilaya zao.

Nao wananchi wa Wilaya hizo wamemshukuru Rais wa Zanzibar kwa uamuzi wake wa kutekeleza miradi hiyo ndani ya Wilaya hizo na kusema kuwa amedhihirisha imani yake kwa wananchi hasa wa kipato cha chini.

“Ni dhahiri kukamilika kwa miradi hii kutapelekea kuondoa kero mbali mbali ziliyopo katika sekta ya elimu na afya na kutunufaisha wananchi ambao uwezo wetu wa kupeleka watoto wetu katika skuli na hospitali za kulipia ni mdogo”, alisema bi. Amina Salum wa Mbuzini.

Kwa upande wao wahandisi wa ujenzi wa miradi hiyo walimueleza Mkuu wa Mkoa kuwa kwa ujumla hadi sasa miradi hiyo inaendelea vizuri na wanatarajia kuikamilisha kwa wakati.  Wamesema kuwa wamekuwa wakipata mashirikiano mazuri kutoka taasisi mbali mbali husika katika kutatua changamoto zinazojitokeza.

Kupitia fedha za  COVID, Mkoa Mjini Magaribi unatarajiwa kunufaika na miradi mbali mbali katika sekta ya afya, elimu, barabara za ndani pamoja na mikopo na majengo ya biashara kwa wajasiriamali ndani ya mkoa huo.