Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewashukuru wafadhili waliojitokeza kuwasaidia wananchi katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Shukurani hizo amezitoa baada ya kukabidhi sadaka ya vyakula kwa wananchi wenye mahitaji maalum kutoka Wilaya tatu za Mkoa Mjini Magharibi, shughuli iliyofanyika katika uwanja wa mnara wa kumbukumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo Kisonge.
Ameeleza kufarahishwa kwake na namna wafadhili hao walivyoitikia wito wake wa kuwasaidia wananchi hasa wenye hali duni na kusema kuwa wamekuwa wakitoa sadaka hiyo kwa wananchi wa Mikoa yote ya Zanzibar kila mwaka.
Aidha Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaangalia namna ya kuwasaidia wananchi waliowengi zaidi katika kipindi kipindi kama hiki cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa miaka ijayo.
Naye Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Mustafa Kitwana amemshukuru Rais wa Zanzibar kwa kukabidhi sadaka hiyo na kueleza kuwa ameonesha ni jinsi gani alivyo na upendo kwa wananchi wake.
Mmoja ya wananchi waliopewa sadaka hiyo Jamila Borafia Hamza akizungumza kwa niaba ya wenzake amemshukuru Rais wa Zanzibar kwa kuwapa kipaumbele watu wenye ulemavu na kuwapatia sadaka hiyo.
Jumla ya wananchi 300 walipewa sadaka wakiwemo walemavu, mayatima, wazee, wajane na watu wanaoishi katika mazingira magumu.