OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Walimu wakuu watakiwa kuhakikisha matokeo mazuri mtihani kidatu cha sita 2024
HabariHabari Mpya

Walimu wakuu watakiwa kuhakikisha matokeo mazuri mtihani kidatu cha sita 2024

Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari za Mkoa Mjini Magharibi wametakiwa kuhakikisha wanafunzi wa kidatu cha sita wanafaulu vizuri katika mitihani yao ya  taifa wanayotarajia kuanza tarehe 6 Mei, 2024.

Akizungumza katika kikao na Walimu hao hapo Afisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Katibu Tawala Mohammed Ali Abdalla amesema uongozi wa Mkoa  usingependa kuona baadhi ya wanafunzi wanapata daraja la nne au zero katika mitihani hiyo.

Akizungumzia kuhusu masomo ya sayansi, Mohamed amesema bado ufaulu kwa masomo hayo sio mazuri na kuwataka walimu hao kuweka mikakati na mbinu zitakazowasaidia wanafunzi kuweza kufanya vizuri katika masomo ya sayansi huku wakizigatia kuwa taifa lina uhutaji mkubwa wa vijana wa fani hiyo.

Katibu Tawala amewataka pia walimu wakuu kuwaelimisha wanafunzi kujiepusha na vitendo vya udanganyifu katika mitihani hiyo kwani vitendo hivyo vitaweza kuwaharibia na kuchafua jina la Mkoa.

Kwa upande mwengine Mohamed ameshauri kuangalia uwezekano wa kuwarudisha darasa wanafunzi wa kidatu cha tano watakaoshindwa kufanya vizuri katika mitihani yao ya kuingia kidatu cha sita.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuwajengea uwezo Ili waweze kufaulu vizuri katika mitihani yao ya taifa ya kidatu cha sita.

Vilevile alisema idadi ya wanafunzi wa kidatu cha nne na sita wanaoacha skuli bado ni kubwa hivyo amewasisitiza walimu hao kuchukua kila juhudi ili kudhibiti vitendo hivyo.

Wakichangia katika kikao hicho walimu hao wamesema kutokana na mikakati waliyoiweka wanamatumaini ya kuja na matokeo mazuri katika mitihani ya mwaka huu.

Naye Afisa elimu Mkoa Mjini Magharibi Mohammed Abdallah Mohammed amesema jumla ya wanafunzi 2,635 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kidatu cha sita katika Mkoa Mjini Magharibi kwa mwaka huu