Wafanyakazi wa umma wametakiwa kutoa mashirikiano yao kwa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF), ili mfuko huo uweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Ushauri huo umetolewa na Kaimu Mkurugnzi Mkuu wa ZHSF Yassir Ameir Juma kwenye kikao chake na wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi kuzungumzia masuala mbali mbali juu ya mfuko huo .
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa hapo Vuga, Yassir amefahamisha kuwa tarehe 20 mwezi huu ndio itakuwa tarahe ya mwisho ya usajili wa wafanyakazi wa umma, hivyo amewataka wafanyakazi wa Ofisi hiyo kukamilisha usajili wao kabla ya tarehe hiyo.
Ameongeza kuwa ZHSF itaanza rasmi kutoa huduma kwa wanachama wake kuanzia mwezi wa Octoba 2023 katika vituo vya afya na Hospitali mbali mbali katika Mikoa yote ya Zanzibar.
Aidha amesema kwamba Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar unaendelea na mazungumzo na taasisi husika ili kuona wanachama wa mfuko huo wanaweza kutumia kadi zao kupata matibabu katika hospitali za Tanzania bara.
Kaimu Mkurugenzi huyo ameeleza pia ZHSF itakuwa ikifanya zoezi la ufuatiliaji na kukagua huduma zinazotolewa katika vituo vya afya na Hospitali ili kuhakikisha wanachama wake wanapata huduma bora.
Amewaeleza wafanyakazi hao kuwa dhamira ya Serekali kuanzisha mfuko huo ni kuhakikisha kuwa wananchi wote wa Zanzibar wanapata huduma bora za afya pamoja na kuwapunguzia mzigo wa kutumia gharama kubwa kulipia matibabu pale wanapopata maradhi mbali mbali.
Naye Katibu Tawala Mkoa Mjini Magharibi Moh’d Ali Abdallah amewataka wafanyakazi hao kuitumia taaluma walioipata kwa kuwaelimisha wafanyakazi wenzao wa umma kuhusu mfuko huo.
Kwa upande wao wafanyakazi wa Ofisi hiyo wameuomba uongozi wa ZHSF kuhakikisha kuwa huduma zitakazotolewa katika hospitali ambazo watakuwa wakipatiwa matibabu zinakuwa bora kwa upande wa madaktari, vipimo na madawa.