Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kuendelea kujenga miundombinu bora ya majengo ya Skuli ili kuboresha huduma za elimu nchini.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Lela Mohammed Mussa amesema hayo katika hafla ya utiaji saini ya mkataba na kukabidhi kazi ya ujenzi kwa kampuni ya FUCHS, hapo Skuli ya Muungano.
Amewataka wakandarasi kuhakikisha wanajenga Skuli yenye ubora na kiwango cha hali ya juu pamoja na kumaliza kwa wakati kwa kuzingatia makubaliano ya mkataba huku akisisitiza umuhimu wa kuwapatia nafasi za kazi vijana wazalendo katika ujenzi wa mradi huo.
Akitoa ufafanuzi juu ya wanafunzi wanaosoma Skuli hiyo ya Muungano, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amesema baadhi ya wanafunzi watahamishiwa kwa muda katika Skuli ya Sebleni na wanafunzi wengine watasoma katika Skuli ambazo zipo karibu na makaazi yao .
Amesema kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi, Skuli hiyo yenye madarasa 13 itavunjwa na kujengwa yenye madarasa 41 ili kukidhi mahitaji pamoja na kupunguza tatizo la wanafunzi wa eneo hilo kufuata masomo Skuli za mbali .
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Muungano Ali Maulidi amesema skuli hiyo ina idadi kubwa ya wanafunzi ambapo darasa moja lina zaida ya wanafunzi 100 jambo ambalo linashusha kiwango cha ufaulu wa wanafunzi, Hivyo ameishukuru Serikali pamoja na Wizara ya Elimu kwa uamuzi wao wa kujenga Skuli hiyo.
Skuli hiyo ya ghorofa tatu itakapo kamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafumzi 1,845 na inatarajiwa kuanza ujenzi wake April 2023 na kumalizika Novemba 2024 ikiwa ni mojawapo ya Skuli 21 zitakazojengwa Zanzibar.