Viongozi na wafanya kazi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Magharibi ‘B’ wamepongezwa kwa mashirikiano yao waliyoyaonesha ambayo yamepelekea Wilaya hiyo kupata ushindi wa kwanza Kanda ya Zanzibar katika Mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka 2024.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa alipokuwa akizungumza na wananchi katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘B’ Mwanakwerekwe mara baada ya mapokezi ya viongozi wa watendaji wa Mkoa huo wakitokea Mkoa wa Mwanza ambapo walihudhuria kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Amewaeleza wananchi waliyohudhuria sherehe hiyo kuwa Wilaya za Mkoa Mjini Magharibi zitaendelea kufanya vizuri katika Mbio za Mwenge wa Uhuru miaka ijayo kutokana na miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea kutekeleza ndani ya Mkoa huo pamoja na muamko wa wananchi kushiriki kwenye Mbio hizo.
Aidha amewashukuru vijana na makundi mbali mbali wakiwemo madereva wa bodaboda na bajaji kwa namna walivyohamasika kushiriki katika mbio za safari hii kitendo ambacho kimechangia ushindi kwa Wilaya hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘B’ Hamida Mussa Khamis amesema mafanikio hayo yametokana na mashirikiano makubwa yaliopo baina ya viongozi wa Wilaya na Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Dimani Kichama.
Kadhalika Mkuu huyo wa Wilaya amewataka vijana hasa wanafunzi huifahamu falfasa ya Mwenge wa Uhuru na kuendelea kuuenzi kama moja ya tunu ya Taifa la Tanzania.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Dimani Kichama Hussein Ali Kimti amesema CCM kama ndio chama kilichoiweka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar madarakani inajivunia ushindi huo.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘B’ Hamida Mussa Khamis akiambatana na watendaji mbali mbali walipokelewa katika Bandari ya Malindi wakiwa na kombe la ushindi.