OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Skuli ya Muungano kujengwa ya horofa 3
HabariHabari Mpya

Skuli ya Muungano kujengwa ya horofa 3

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inatarajia kuanza  hivi karibuni ujenzi wa Skuli ya horofa tatu ya Muungano katika Wilaya ya Mjini.

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amesema hayo alipokuwa akizungumza na Walimu hapo  wa Skuli ya Msingi Muungano kuhusu ujenzi huo.

Amesema  madarasa yanayotumika sasa yatavunjwa ili kuruhusu ujenzi wa Skuli hiyo mpya ambayo itakuwa ya kisasa, hivyo  amewataka walimu kuliunga mkono suala la ujenzi wa skuli  hiyo pamoja na kutoa ushirikiano wao.

Amewahakikishia walimu kuwa ujenzi utakapomalizika Skuli hiyo itaendelea kuwa ya msingi na watarudi mahala hapo pamoja na wanafunzi wao ili waweze kuendelea na masomo.

Mkuu wa Mkoa amesema lengo  ya Serikali ya awamu ya nane ni kuondokana na madarasa ya chini na kujenga majengo ya horofa katika Skuli zote nchini ili kuboresha mazingira ya ufundishaji, kupunguza idadi ya wanafunzi madarasani na kuwa na mkondo mmoja wa kuingia Skuli.  

Aidha Mhe. Idrissa ameeleza kuwa Serikali iko mbioni kuanza ujenzi wa Skuli tano za horofa na moja ya ufundi katika Mkoa Mjini Magharibi hatua ambayo itapunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya madarasa yanayohitajika katika Mkoa wake.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa amezungumzia juu ya suala la vitendo vya udhalilishaji na kuwataka walimu kuwa karibu na wanafunzi  pamoja na kuwafuatilia nyendo zao ili kuwaepusha na vitendo hivyo.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Wazazi  Mbwana Khamis Mbwana   ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake wa kujenga jengo la horofa la Skuli hiyo ya Muungano.

Jumla ya madarasa mapya  2000 yanahitajika  katika Mkoa Mjini Magharibi ili kuweza kuwa na idadi ya wanafunzi 40 kwa kila darasa sambamba na kupunguza mikondo miwili ya kuingia Skuli.