Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa ameuagiza uongozi wa Wakala wa Barabara Zanzibar kuchukua hatua za dharura kuifanyia matengezezo barabara itokayo Kinuni Skuli hadi Fuoni Mambosasa ili kuwaondoshea usumbufu wakaazi wa maeneo hayo.
Agizo hilo amelitoa huko Kinuni akiwa pamoja na viongozi wa Wilaya, Manispaa Magharibi ‘B’ na Wakala wa barabara walipofika kukagua barabara hiyo pamoja na kuzungumza na wananchi.
Amewafahamisha wananchi hao kuwa Serikali imekusudia kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami hata hivyo wakati ikisubiri mradi huo kutekelezwa barabara hiyo itawekwa kifusi ili iweze kupitika kwa urahisi.
Mkuu wa Mkoa amesisitiza kwamba Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi inadhamira ya dhati ya kuimarisha huduma zote muhimu za kijamii ikiwemo elimu, afya na miundo mbinu mbali mbali na kuwataka wananchi hao kuendelea kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na Serikali yao.
Aidha Idrissa amewahimiza viongozi wa Majimbo na Wadi kuzipatia ufumbuzi changamoto ndogo ndogo zinazowakabili wananchi pamoja na kusimamia utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi kwenye maeneo yao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘B’ Hamida Mussa Khamis amewataka wakaazi wa maeneo hayo kuacha kujenga kando ya barabara ili kuepusha kuvunjiwa wakati barabara hiyo itakapojengwa.
Nae Mkurugenzi wa Idara ya Utunzaji wa barabara Mhandisi Safia Juma amesema kuwa tayari wameshaifanyia ukaguzi wa kitaalamu barabara hiyo na wanasubiri kupata fedha ili kuanza na ujenzi wa mtaro na kuweka kifusi kwa hatua ya awali.
Wakaazi wa Kinuni wamemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa uamuzi wake wa kuikagua barabara hiyo pamoja na maagizo yake aliyoyatoa ya kuifanyia matengenezo.