Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezindua Mpango Mkakati pamoja na mradi wa Tumaini wa kuzalisha taulo za wasichana kwa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF).
Uzindizi huo umefanyika kwenye maadhimisho ya mwaka moja tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo huko katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, Kiembe Samaki.
Ameeleza kufurahishwa kwake na kazi nzuri inayofanywa na Taasisi hiyo na kuipongeza kwa jithada zake za kuiunga mkono Serikali katika kuinua juhudi za kina mama na vijana wanaojishuhulisha na Kilimo cha Mwani kwa kuwapatia mafunzo pamoja na vifaa.
Aidha Dkt. Mwinyi amezungumzia suala la lishe bora kwa kinamama wajawazito na watoto na kusema takwimu zinaonesha kwa wastani watoto wawili kati ya watoto kumi wamekosa lishe bora jambo ambalo linaweza kuepukika.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini na muanzlishi wa Taasisi ya ZMBF Mama Mariam Mwinyi ameelezea mafanikio walioyapata katika kipindi cha mwaka mmoja kuwa ni pamoja na utekelezaji wa programu mbalimbali ikiwemo Uzalishaji na ugawaji wa Taulo za wasichana, utowaji wa Boti pamoja na Mafunzo ya ujengaji uwezo kwa wakulima wa mwani.
Kadhalika amesema taasisi hiyo imeweza kufanikiwa kutokana na michango ya kifedha, vifaa, pamoja na utaalamu wanaoupata kutoka kwa wadhamini mbali mbali katika kutekeleza programu zake na kutaja baadhi ya mashirika yakiwemo Benjameni Mkapa Foundation, Shirika la Pact, Ubalozi mdogo wa China pamoja na Mashirika mengine.
Akizungumzia kuhusu mipango ya muda mrefu kwa taasisi hiyo Mkurugenzi wa ZMBF Mwanaidi Ali amesema wameandaa Mpago Mkakati wa miaka mitatu ambao utahusisha programu mbalimbali zitakazowahusu Vijana, Kinamama pamoja na makundi mengine ambao unatarajiwa kugharimu kiasi cha shillingi millioni 2 za kimarekani katika utekelezaji wa mkakati huo.
Nae mmoja kati ya wanufaika wa ZMBF Safia Hashim ameeleza namna taasisi hiyo ilivyobadilisha maisha yao kwa kuwapatia msaada wa vifaa wakulima wa mwani ikiwemo boti 17. Aidha ameushukru uongozi wa ZMBF kwa namna wanavyowapatia mashirikiano kila wanapohitaji misaada ya kuendesha shughuli zao
Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation ilianzishwa Julai 2021 na kuzinduliwa rasmi Febuari 2022 na muanzilishi wake Mama Mariam Mwinyi Mke wa Rais wa Zanzibar.