Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Hussein Ali Mwinyi, amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Ugonjwa wa Uviko-19, akibainisha kuwa mbali na ugonjwa huo kuathiri afya za binadamu lakini pia unadhoofisha uchumi wa nchi.
Al Hajj Dk. Mwinyi ametoa tahadhari hiyo katika salamu alizotoa kwa waumini wa dini ya Kiislam mara baada ya ibada ya sala ya Al-Jumaa, iliyofanyika msikiti wa Masjid Mamiali, Mkoa Mjini Magharibi Ungua.Rais Dk. Mwinyi amesema wakati huu Dunia ikiwa katika hatari ya kukabiliana na wimbi la tatu la ugonjwa huo, kuna umuhimu kwa wananchi kuzidisha tahadhari na kubainisha jinsi ugonjwa huo ulivyoathiri pato la Taifa hapa nchini. Aidha Rais, Dk. Mwinyi aliwasihi waumini kumuomba Mwenyezi Mungu ili ugonjwa huo uondoke na hali ya Uchumi ipate kutengemaa.
Katika hatua nyingine, Rais Dk. Mwinyi amesisitiza suala la kuimarisha Umoja na mshikamano katika nchi yetu huku akiweka wazi kuwa, Umoja huleta Amani na Utulivu na Amani ndio msingi wa Maendeleo kwa nchi yoyote.