OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Wakaazi wa Nyumba za Mjerumani Waridhia Ujenzi wa Mji wa Kisasa
HabariHabari Mpya

Wakaazi wa Nyumba za Mjerumani Waridhia Ujenzi wa Mji wa Kisasa

Wakaazi wa Nyumba za Mjerumani ziliopo Kikwajuni wameeleza kuridhishwa na mapendekezo ya Serikali ya kutaka kujenga Mji wa kisasa katika eneo hilo.

Kauli hizo zimetolewa na baadhi ya wakaazi wa Nyumba hizo mara mara baada ya kikao kilichozungumzia mradi huo ambacho kilishirikisha pia uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi na Shirika la Nyumba Zanzibar hapo Afisi ya Mkuu wa Mkoa, Vuga.

Wamesema kikao hicho kimewapa uelewa wa kutosha kuhusu hatua zote zitazokachukuliwa na Serikali katika utekelezaji wa mpango huo hivyo wapo tayari kuwaelimisha wakaazi wenzao ili kupisha mradi huo uweze kuanza.

Aidha wamekiri kuwa nyumba hizo za Mjerumani zipo katika hali mbali kwa sasa inayohatarisha maisha yao na kutoa shukurani zao kwa Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuja na mradi huo.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba Zanzibar Sultan Said Suleiman amewaomba wananchi hao kutumia busara katika kuwaelimisha wakaazi wenzao na vilevile kutoweka vikwazo vitakavyokwamisha mradi huo.

Amewafahamisha kuwa endapo kutakuwa na vikwazo kutoka kwa wakaazi hao Shirika litashindwa kuutekeleza mradi huo na huenda likafikiria kuupeleka mahala pengine.

Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Nene ina nia njema kuhusu mradi huo ambapo lengo ni kuhakikisha wananchi hao wanapata makaazi yaliyo bora baada ya mradi kukamilika.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Katibu Tawala Mohamed Ali Abdalla amewaomba wakaazi wa Nyumba za Mjerumani kuunga mkono mpango huo wa Serikali.

Nyumba za Mjerumani zilijengwa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume mnamo mwaka 1964.