OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>RC Kitwana afanya ziara miradi ya ujenzi wa masoko
HabariHabari Mpya

RC Kitwana afanya ziara miradi ya ujenzi wa masoko

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amewataka  wakandarasi wanaojenga  Soko la Chuini, Jumbi na Mwanakwerekwe kuongeza kasi ya ujenzi ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika mwezi ujao.

Akizungumza mara baada ya kukamilisha ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa masoko hayo matatu akiwa ameambatana na Wakuu wa Wilaya na watendaji mbali mbali, amesema kutokana na hatua iliyofikiwa, Mkoa unamatumaini makubwa kuwa miradi hiyo itaweza kukamilika ndani ya muda uliopangwa.

Mkuu huyo wa Mkoa amewaeleza wakandarasi  Kikosi cha Kujenge Uchumi (JKU), Zimamoto na Chuo cha Mafunzo kuwa lengo la ziara yake pamoja na kukagua hatua ya ujenzi iliyofikiwa vilevile kuweza kuwahimiza  kuongeza kasi ya ujenzi.

Aidha ameeleza kuridhishwa  na hatua ya ujenzi iliyofikiwa na kuvitaka vikosi hivyo kuendelea kuifanya kazi hiyo kwa kiwango kinachotakiwa katika hatua iliyobakia.

Sambamba na hayo  Idrissa ameyaagiza Mabaraza ya Manispaa Magharibi ‘A’ na Magharibi ‘B’ kuanza kuandaa utaratibu mzuri wa kuwaweka wafanyabiashara ili masoko hayo yaweze kutumika kikamilifu na kuleta manufaa kwa wananchi.

Vilevile amewakikishia wafanyabiashara waliokuwepo kwenye maeneo hayo kabla ya ujenzi kuwa watapewa kipaumbele cha kupata nafasi ya kufanya biashara  wakati masoko hayo yatakapofunguliwa.

Meneja Mradi na Mshauri elekezi kutoka Wakala wa Majengo Zanzibar Shadya Fauz Mohammed amesema ujenzi wa masoko yote matatu upo katika hatua za mwisho mwisho na wanatarajia yatakamilika mwishoni mwa mwezi ujao.

Naye Mkuu wa Utawala wa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU), Kanal Haji Ali Ali ambao wanajenga Soko la Manakwerekwe amesema Kikosi chake kimeweka mpango kazi ambao ikiwa watautekeleza vilivyo wataweza kukamilisha ujenzi kwa wakati.

Ujezi wa Soko la Chuini  umefikia asilimia 78, Jumbi 86 na Mwanakwerekwe 80.