Masheha wa Mkoa Mjini Magharibi wametakiwa kuwatumia kikamilifu Polisi Shehia katika kushughulikia changamoto mbali mbali kwenye maeneo yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Polisi Richard Tadeo ametoa ushauri huo katika kikao na baadhi ya Masheha wa Shehia za Wilaya ya Mjini kwa ajili ya kuwasikiliza changamoto ziliomo kwenye Shehia.
Akizungumza katika katika kikao hicho kilichofanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Vuga Kamanda Tadeo amesema Polisi Shehia, Masheha na wananchi wote wana jukumu la kulinda amani na usalama hivyo bila ya mashirikiano itakuwa vigumu kuweza kudhibiti matukio ya kihalifu.
Aidha amewataka wananchi kuchukua hatua za haraka kuripoti vituo vya Polisi pale yanapotokea matukio ya kihalifu katika maeneo yao badala ya kuwaachia Polisi Shehia na Masheha kutoa taarifa za matukio hayo.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa Mjini Magharibi Moh’d Ali Abdalla amesema utaratibu huo wa kukutana na Masheha kusikiliza changamoto ziliomo katika Sehia zao utakuwa endelevu lengo ni kuhakikisha amani na utulivu inaimarika ndani ya Mkoa huo.
Nao Masheha walioshiriki kikao hicho wameomba utaratibu huo uwe ukifanyika mara kwa mara kwa vile utasaidia kupunguza matukio ya kihalifu katika Shehia zao.
Masheha wamezitaja kero kadhaa zinazowakabili ikiwemo vijana wanaojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya na pombe, majengo ya kuuzia pombe, kamari, vitendo vya Udhalilishaji, uharibifu wa mazingira, uhalifu na wahamiaji holela.
Mkoa Mjini Magharibi unajumla ya Shehia 121, Wilaya ya Mjini Shehia 56, Wilaya ya Magharibi ‘A’ Shehia 31 na Wilaya ya Magharibi ‘B’ Shehia 34.