Uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi umeahidi kuwa utachukuwa hatua za haraka kukaa pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ili kuweza kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazozikabili Skuli mbali mbali za Mkoa huo.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa Mjini Magharibi Moh’d Ali Abdalla katika mkutano wake na walimu wakuu wa Skuli za maandalizi, msingi na sekondari zilizomo katika Mkoa huo.
Akizungumza na walimu hao katika ukumbi wa mikutano wa Afisi ya Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala amewahakikishia kwamba Serikali ya Mkoa itashirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ili kuona baadhi ya changamoto walizozieleza zinafanyiwa kazi na kupatiwa ufumbuzi ndani ya muda mfupi.
Akijibu kuhusu changamoto ya uhaba na uchakavu wa madarasa, Moh’d amewaomba walimu wakuu hao kuwa wastahamilivu katika kipindi hiki ambacho Serikali imekuwa ikiendelea na ujenzi wa majengo mapya ya Skuli za horofa katika maeneo mbali mbali ya Mkoa Mjini Magharibi.
Amesema mbali na ujenzi unaoendelea wa Skuli saba za horofa kwenye Mkoa huo, Serikali ina mpango pia wa ujenzi wa Skuli nyengine mpya pamoja kuzifanyia ukarabati mkubwa skuli zilizo chakavu ili kuondokana kabisa na tatizo la uhaba wa madarasa.
Kuhusu changamoto ya vitendo vya utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wanafunzi, Katibu Tawala amesema suala la kuzingatia nidhamu kwa wanafunzi halina mbadala na kuwataka walimu hao kuwa na msimamo katika kusimamia misingi ya kazi yao.
Amewaeleza kuwa pamoja na jukumu lao la kutoa elimu vile vile wanawajibu wa kuisaidia serikali katika kuwajenga vijana wenye nidhamu na maadili mema kwa maslahi ya taifa la sasa na kizazi kijacho.
Wakizungumzia juu ya changamoto zinazowakabili walimu hao wameeleza kuwa bado wamekuwa wakikabiliwa na uhaba wa madarasa hali inayopelekea wanafunzi kusoma katika mazingira magumu, uchakavu wa madarasa, ukosefu wa vikalio, upungufu wa walimu na wahudumu.
Aidha wametaja changamoto nyengine ni mazingira yasiyo rafiki kwa wanafunzi kutokana na vitendo vya wizi, uhalifu na matumizi ya madawa ya kulevya katika maeneo yanayozunguka skuli.
Wameiomba Serikali ya Mkoa kushirikiana na Wizara ya Elimu kufanya tathmini ya Skuli zilizo chakavu ili waweze kuzipa kipaumbele kuzifanyia ukarabati wa haraka Skuli ambazo zipo katika hali mbaya zaidi.
Wameushukuru uongozi wa Mkoa kwa kuona umuhimu wa kukutana na walimu wakuu wa Skuli za Serikali kutoka Wilaya tatu za Mkoa Mjini Magharibi kusikiliza changamoto zao.
Kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa Mjini Magharibi Mohammed Abdalla Mohammed amesema katika kipindi cha miaka miwili cha Serikali ya awamu ya nane jumla ya madarasa 394 yamejengwa katika Mkoa Mjini Magharibi.
Amesema kwa sasa mkoa unakabiliwa na upungufu wa madarasa 842 ambapo idadi hiyo itapungua kwa kiwango kikubwa baada ya kumalizika kwa ujenzi wa Skuli saba za horofa zinazotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.