Makamo wa Kwanza wa Rais Mhe. Othman Masoud Othman amewahimiza watendaji na wafanyakazi wa Mabaraza ya Manispaa na Wilaya ya Mjini, Magharibi A na Magharibi B kuongeza juhudi katika kutunza mazingira pamoja na upandaji wa Miti.
Amesema hayo huko Skuli ya Abuod Jumbe Fuoni na Ukumbi wa Studio za Redio Rahaleo alipokuwa akizungumza na watendaji hao kwa nyakati tofauti kuhusu mpango wa Serikali unaojulikana kama Zanzibar ya Urithi wa Kijani.
Amesema kutokana na athari za kimazingira zinazoikabili Zanzibar kwa sasa ikiwemo uharibifu wa vianzio vya maji, kupotea kwa miti ya asili na viumbe mbali mbali na ujenzi katika maeneo ya kilimo, Serikali imeamua kuja na mpango huo ili kuepusha athari zaidi hapo baadae.
Makamu wa Rais amesisitiza suala la ushirikiano katika kutunza mazingira na kuwataka watendaji kuwahamasisha wananchi kuwa na utamaduni wa kupanda miti katika maeneo yao badala ya kuikata kwa sababu zisizo za msingi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B Mhe. Hamida Mussa Khamis amesema licha ya juhudi kubwa wanazochukuwa kuhifadhi mazingira, bado Wilaya zao zinakabiliwa na changamoto ya uchimbaji wa kifusi, mawe, na mchanga katika baadhi ya Shehia.
Amemueleza Makamu wa Kwanza wa Rais kwamba Wilaya zitashirikiana na Sekta zote husika ili kuona mpango wa Zanzibar ya Urithi wa Kijani unafanikiwa kupitia programu mbali mbali watakazozitekeleza za upandaji wa miti.
Awali Wakurugenzi wa Mabaraza ya Manispaa waliwasililisha taarifa zao za utekezaji wa kazi kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2022 na kueleza mafanikio na changamoto zilizopo ikiwemo muamko mdogo kwa wananchi katika suala la kutunza mazingira, kuengezeka kwa uzalishwaji wa taka na baadhi ya wananchi kutolipa ada ya taka.