Wafanyabiashara wa Mkoa Mjini Magharibi wamehimizwa kukata bima ili iweze kuwasaidia pale zinapotokea changamoto mbali mbali katika biashara zao.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe.Idrissa Kiwana Mustafa katika hafla ya uzinduzi wa kampeni ya Benki ya NMB ya “UmeBIMA” iliyofanyika Darajani, Wilaya ya Mjini.
Amesema bado wafanyabiashara wengi hasa wadogo wadogo hawana muamko katika kukata bima, hivyo amewataka wabadilike ili wanufaike na fursa za bima zinazotolewa na Benki ya NMB na makampuni mengine mbali mbali katika Mkoa wake.
Amewapongeza Benki ya NMB kwa kuja na kampeni hiyo ya kuhamasisha ukataji wa bima mbali mbali na kuwataka kuendelea kutoa elimu juu ya suala hilo ili iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Kwa upande mwengine Mkuu wa Mkoa amewahakikishia wafanyabiashara kuwa Serikali itaendendelea kuwajengea mazingira mazuri ya shughuli zao kwa ujenzi wa masoko na vituo vya biashara kwenye Wilaya zote za Mkoa huo.
Amewataka waendelee kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi za kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.