Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini Mchango wa Mashirika ya Serikali na Binafsi katika Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi Katika kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa maendeleo ya Zanzibar.
Mhe. Hemed ameeleza hayo katika Hafla ya Uchangiaji wa Rasilimali za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 iliyofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutambua umuhimu wa Mashirika hayo kwa kuwashirikisha moja kwa moja katika Suala la uchangiaji wa Rasilimali za kufanikisha Zoezi hilo.
Mhe. Hemed ambae pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi amesema uhitaji wa Vifaa na Rasilimali Fedha Jumuiya ya Wafanyabiashara, Asasi za Kiraia na Wadau Wengine wamekuwa Mstari wa mbele kwa kuiunga Mkono Serikali kwa kuleta Mchango mzuri katika utekelezaji wake.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameeleza kuwa Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi lina umuhimu Mkubwa kwa kuiwezesha Serikali na wadau mbali mbali kupata Hisabu halisi ya Idadi ya Watu Nchini pamoja na Taarifa zao za Kijamii, kiuchumi na Makazi yao.
Aidha ameeleza kuwa matokeo yatakayopakana katika Sensa yatasaidia kupata Takwimu Sahihi katika kufanya Maamuzi ya kuleta Maendeleo ya Taifa.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed amewahakikishia Wadau hao kuwa Rasilimali zitakazokusanywa zitatumika ipasavyo kama ilivyokusudiwa ili kufanikisha Zoezi hilo kwa ufanisi wa Hali ya juu.
Nae Waziri wa Nchi Afisi Ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe. Hamza Hassan Juma ameeleza kuwa Uelewa wa Wananchi kuhusu Sensa ni Mkubwa kutokana na Uhamasishaji uliofanywa tokea mwanzo wa Mwaka huu hatua ambayo inaashiria kukamilika vyema Zoezi hilo.
Nae Mkurugenzi Mtendaji Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar Ndg. Hamad Hamad ameeleza kufurahishwa kwa kushirikishwa katika Hatua zote za Maandalizi ya Sensa mwaka huu na kueleza kufurahishwa kwao kuona kuwa zoezi hilo kwa Mwaka huu litarahisisha Wananchi kupata Biashara kirahisi kwa kutumia Mfumo wa Anwani za Makazi.