OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>RC-Kitwana “Elimu ya Kilimo hai itolewe kwa Wakulima”
HabariHabari Mpya

RC-Kitwana “Elimu ya Kilimo hai itolewe kwa Wakulima”

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amewataka washiriki wa kongamano la kilimo kuwaelimisha wakulima juu ya umuhimu wa kutumia njia za asili katika  kilimo badala ya matumizi ya mbolea zenye kemikali.

Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo wakati akifunga kongamano kuhusu  kilimo hai yaliofanyika Hoteli ya  Ngalawa  Kihinani, Wilaya ya Magharibi A.

Amesema kwamba tafiti zinaonesha kuwa matumizi ya mbolea za kemikali yana athari kubwa kwa afya za watu na mazingira  na kusema kuwa wakati umefika kwa wakulima kurudi katika kilimo cha zamani pamoja na kutumia mbolea za asili.

Mkuu wa Mkoa ameipongeza Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji na Mifugo kwa kuona umuhimu wa kuwaelekeza wakulima katika kilimo cha kutumia njia za asili hatua ambayo itasaidia pia jamii kuepukana na athari mbali mbali zitokanazo na matumizi ya mbolea za kemikali.

Aidha amewataka washiriki wa kongamano hilo kuitumia elimu waliyoipata kwenda kuwaelimisha wakulima ili  nao waweze kupata  uwelewa kuhusu kilimo hai.

Idrissa ameishauri Wizara ya Kilimo kuendelea na program za aina hiyo ili kufikisha elimu inayohusu kilimo hai kwa wakulima wengi zaidi  wa Mkoa wa Mjini Magharibi na Mikoa Mingine.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji na Mifugu ndugu Said Shaaban amesema Wizara yake imeona kuna umuhimu mkubwa wa kujielekeza kwenye kilimo hai kutokana na tija mbali mbali zitokanazo na kilimo hicho.  

Kongamano hilo la siku mbili liliendeshwa na Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji na mifugo kwa kushirikiana na   Agri – Connect, lilifunguliwa na Waziri wa Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Riziki Pembe Juma kwa niaba ya Waziri wa Kilimo.