Uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi umeahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Makamu wa Pill wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla .
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa wakati wa ziara ya Makamu Makamu wa Pili wa Rais Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla alipofanya ziara ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo inayojengwa kwa fedha za UVIKO 19 katika Wilaya ya Magharibi A.
Amemueleza Makamu wa Pili kuwa uongozi wa Mkoa utakaa pomoja na sekta husika ili kujadili changamoto zilizojitokeza kwenye baadhi ya miradi na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka . Kwa upande mwengine Mkuu wa Mkoa amekipongeza Kikosi cha Kujenga Uchumi JKU na Kampuni ya CRJE kwa kuendelea vizuri na ujenzi wa miradi waliopewa.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais alieleza kutoridhishwa na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Monduli na kuitaka Wizara ya Elimu kusimamia mkataba wa ujenzi ili kuhakikisha mradi huo nao unamilika kwa wakati uliokusudiwa.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Lela Mohammed Mussa amesema Wizara itachukua hatua kwa mujibu wa mkataba dhidi ya mkandarasi na kumhakikishia Makamu wa Pill kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati.
Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais alikagua ujenzi wa Skuli, Soko la wajasiriamali Monduli na Hospitali ya Wilaya ya Magharibi A iliopo Mbuzini.