Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amesema yapo maeneo mbali mbali ambayo Mkoa huo utaweza kushirikiana na Mkoa wa Zhejiang kupitia uhusiano uliyoanzishwa.
Amesema hayo alipokuwa na mazungumzo na Naibu Mkuu wa Mkoa wa Zhejiang kutoka China Yang Qingjiu alipofika Ofisini kwake Vuga kumsalimia akiambatana na viongozi mbali mbali.
Ametaja moja ya eneo ambalo Mkoa wake utaweza kushirikiana nao ni katika suala la teknolojia na mifumo ya ulinzi, usafiri, ukusanyaji wa mapato na shughuli nyengine za Serikali kwa vile China imepiga hatua kubwa katika teknolojia.
Aidha amesema eneo jengine ni mashirikiano ya kibiashara kati ya Mikoa hiyo miwili kwa kuwapatia soko wajasiriamali wa Mkoa huo kuuza bidhaa zao nchini China na wafanyabiashra kutoka China kuleta bidhaa zao Zanzibar.
Kwa upande Mwengine Mkuu wa Mkoa amewakaribisha wawekezaji kutoka Zhejiang kuja kuwekeza katika Mkoa Mjini Magharibi katika sekta ya utalii, uvuvi, uchumi wa buluu na viwanda.
Amemshukuru kiongozi huyo pamoja na ujumbe kwa kuamua kuja Zanzibar kuanzisha mashirikiano hayo na kusema kuwa atahakikisha yanazidi kuimarika kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Akizungumzia kuhusu ujio huo, Meya wa Jiji la Zanzibar Mstahiki Mahmoud Mohamed Mussa amesema watazitumia vizuri fursa zote zitakazopatikana kupitia uhusiano huo pamoja na kuyafanyia kazi maeneo yote yaliyoainishwa kushirikiana.
Naye Naibu Mkuu wa Mkoa wa Zhejiang Yang Qingjiu amesema kuwa wapo tayari kuusaidia Mkoa Mjini Magharibi kwa kuwapatia mafunzo na utaalamu katika suala la ulinzi na mifumo ya mawasiliano.
Ametaja maeneo mengine ambayo watashirikiana na Mkoa huo ni pamoja na kuboresha utendaji kazi wa Mabaraza ya Manispaa sekta ya biashara, michezo na huduma nyengine za kijamii.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Kamishna Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar CP Hamad Khamis Hamad.