OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA IDARA MAALUM ZA SMZ

OFISI YA MKUU WA MKOA MJINI MAGHARIBI

Home>>Habari>>Dk.Stergomena Tax amesisitiza kuendeleza mashirikiano baina ya Kamati za Usalama na Vikosi vya SMZ
HabariHabari Mpya

Dk.Stergomena Tax amesisitiza kuendeleza mashirikiano baina ya Kamati za Usalama na Vikosi vya SMZ

Waziri wa Ulinzi na  Jeshi la Kujenga Taifa Dk.Stergomena Tax amesisitiza kuendelezwa  mashirikiano yaliopo baina ya Kamati za Usalama za Mikoa na Vikosi vya Ulinzi ili kuimarisha amani na utulivu iliopo nchini.

Ushauri huo ameutoa wakati alipokutana na Kamati ya Usalama ya Mkoa Mjini Magharibi alipofika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo Vuga akiwa katika ziara yake hapa Zanzibar.

Amesema uhusiano na mashirikiano kati ya vyombo hivyo ni jambo la muhimu sana hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto kubwa ya vitendo vya ugaidi na uhalifu wa kimtandao.

Waziri wa Ulinzi amewataka viongozi wa Mikoa kuendelea kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na Viongozi Wakuu wa Nchi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kubaki kuwa na amani na uchumi uliyo imara.

Amesema bila ya amani hakuna linaloweza kufanikiwa na kusema kwamba viongozi hao wanawajibu wa kulisimamia suala hilo ili Serikali zote mbili ziweze kutekeleza mipango yake ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Aidha Dk. Stergomena ameupongeza uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kusimamia amani ndani ya Mkoa huo na kuwahakikishia kuwa Wizara yake itawapa kila mashirikiano ili Kamati za Usalama za Mikoa ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanizi zaidi.

Naye Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Mkoa huo, Idrissa Kitwana Mustafa amemueleza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuwa kumekuwepo na mashirikiano makubwa kati ya Serikali ya Mkoa na Vikosi vyote vya Ulinzi nchini.

Amesema kutokana na mshirikiano hayo hali ya usalama ndani ya Mkoa wake ipo vizuri jambo linalopelekea wananchi wa Mkoa huo kuweza kuendelea na shughuli zao za maisha kama kawaida.

Ameongeza kuwa Mkoa unaendelea kupambana na vitendo vya uhalifu, udhalilishaji na matendo yote ya uvunjifu wa sheria kupitia vyombo vya ulinzi na usalama.

Mkuu wa Mkoa amemueleza Waziri wa ulinzi kuwa mbali na suala la ulinzi Serikali ya Mkoa inaendelea kusimamia na kutekeleza maagizo na maelekezo ya Viongozi Wakuu wa Serikali zote mbili.